Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea taarifa
kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), mnamo tarehe 19 Oktoba 2017 kuhusu
ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda tangu
tarehe 17 Octoba, 2017. Maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huo ni Wilaya
ya Kween, Kanda ya Mashariki ya nchi, ambayo inapakana n nchi ya
Kenya. Hadi kufikia tarehe 19 Oktoba 2017, watu 4 walikwishapata
maambukizo ya ugonjwa huo, ambapo wawili kati yao wamepoteza maisha.
Wizara
inatoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi katika mikoa yote ya
Tanzania, hususan kwa wale wanaoishi katika mikoa ambayo inapakana na
na nchi ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza na Kagera).
Ugonjwa
wa Marburg unafanana sana na ugonjwa wa Ebola. Virusi vinavyosababisha
ugonjwa wa Marburg vinajulikana kama “Marburg Virus”, navyo vipo
katika jamii moja na virusi vinavyosababisha Ebola (Ebola virus).
Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa
za Virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini, (Viral Haemorrhagic
Fevers). Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.
Dalili
kuu za ugonjwa huu ambazo huanza ghafla ni pamoja na Homa kali, maumivu
makali ya kichwa pamoja na mwili kuishiwa nguvu ambapo baadaye
huambatana na kuharisha sana (majimaji), maumivu ya tumbo, kichefuchefu
na kutapika na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia
ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali inayopelekea
kifo kwa muda mfupi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati
ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.
Ugonjwa
huu unaenea kwa urahisi sana na haraka kutoka mtu mmoja hadi mtu
mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana na mate, damu,
mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na
jasho au kumgusa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg. Ugonjwa huu pia
unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa wa
Marburg.
Wizara ya Afya , imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:
Kutoa
taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na
Wilaya kupitia OR-TAMISEMI. Taarifa hiyo imejumuisha namna Ukweli
kuhusu ugonjwa (Fact sheet),
Kuimarisha
ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa,
Wilaya na maeneo ya mipaka ya nchi kavu na maji. Aidha watalaamu hawa wa
Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili
endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema na
kushughulikiwa.
Vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya na vipima joto maalum (thermoscan) tayari vipo katika maeneo husika ya mikoa.
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote wa
Marburg aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa
kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa
yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Kitengo cha mawasiliano ya Serikali
30/10/2017
0 comments: