Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino
Mlowola amemtahadharisha Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua
Nassari kuacha kugeuza taarifa anazoziwasilisha kwenye taasisi hiyo kuwa
ni za kisiasa.
Mlowola
ametoa tahadhari hiyo kwa Nassari leo Jumanne, Oktoba 17, 2017
alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema endapo Nassari ataendelea kuingiza siasa kwenye suala hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mlowola
amesema kitendo cha mwanasiasa huyo kuweka hadharani taarifa za
uchunguzi ni kinyume cha sheria kwa kuwa kazi hiyo inatakiwa kufanyika
kwa siri na Mahakama ndiyo yenye jukumu la kuchukua hatua.
Amesema
Takukuru ina wajibu wa kumlinda mtoa taarifa lakini jukumu hilo
linakuwa tofauti kwa Nassari ambaye ameamua kujitokeza hadharani.
"Alicholeta
Nassari kwetu ni taarifa si ushahidi. Ameleta tumezipokea na
tunazifanyia kazi, inashangaza anapozungumza na vyombo vya habari na
kutuelekeza namna ya kufanya kazi," amesema.
Mlowola
amesema, "Tulishampa angalizo kuwa mambo tunayoongea ni siri lakini
mwenzetu inaonekana anafanya siasa kama anavyosema mwenyewe kuwa
ataendelea kuleta ushahidi kama series ya Isidingo."
Mkurugenzi
mkuu huyo amemtaka Nassari kuacha kukiingiza chombo hicho kwenye siasa
ili kifanye kazi kwa uhuru kama sheria inavyoelekeza.
"Nitoe
rai kwa Nassari na wengine wote, ukishaleta taarifa kwenye chombo
husika kama hiki kiache kifanye kazi. Hakuna sababu ya kukishinikiza au
kukiingiza kwenye malumbano ya kisiasa. Ukweli wa mambo utajulikana
mahakamani," amesema.
0 comments: