SEKRETARIETI
ya Ajira katika Utumishi wa Umma imebainisha kuwa bado kuna baadhi ya
waombaji wa kazi za utumishi wa umma wanaoendelea kughushi sifa za
kielimu, taaluma na taarifa binafsi pamoja na hatua kali zinazoendelea
kuchukuliwa na serikali.
Kutokana
na taarifa hiyo, serikali imeagiza sekretarieti hiyo kufungua kanzi
data ya kutengeneza orodha ya watu wote wanaoomba ajira kupitia chombo
hicho watakaobainika kufanya udanganyifu kupitia vyeti vyao ili wawekewe
zuio la ajira za utumishi wa umma serikalini.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angella Kairuki aliagiza sekretarieti hiyo kuwachukulia hatua waombaji
wote watakaobainika kuwasilisha taarifa za taaluma zenye udanganyifu
ikiwa ni pamoja na kuanzisha kanzidata yenye orodha yao ili wawekewe
zuio la ajira serikalini.
“Naomba
utaratibu uwekwe wa kuwasajili watu hawa wadanganyifu kupitia kanzidata
na kuwa ‘black listed’ (kuwafungia), orodha hii ipelekwe kwenye ofisi
zote na taasisi zote za serikali ili wasipate ajira kwa njia yoyote,
lakini pia washitakiwe kwa kuthubutu kuja kwenye chombo kizito kama hiki
na kudanganya,” alifafanua Kairuki.
Aidha,
imebainika kuwa baada ya ajira kufunguliwa katika mwaka wa 2017/18,
sekretarieti hiyo imepokea vibali vya ajira 292 vyenye jumla ya idadi ya
nafasi 2,611 na hadi kufikia Septemba mwaka huu, waombaji 185
wameshapangiwa vituo vya kazi.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa bodi mpya na Mkataba wa Huduma kwa Mteja ya
Sekretarieti hiyo ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Katibu wa
Sekretarieti hiyo, Xavier Daudi alisema kughushi vyeti bado ni
changamoto wanayoendelea kukumbana nayo.
Daudi
alisema pamoja na chombo hicho kimeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja
na kufuatilia vyeti hivyo vya kughushi vinapotolewa na kwamba imebaini
taasisi zinazotambulika zinazotoa vyeti hivyo.
“Hili
tumeliona hasa kwenye nafasi za udereva, kuna vyuo vya udereva vya
mitaani tena vilivyosajiliwa na Vyuo Ufundi vya Veta, tulipofuatilia na
kuvihoji baadhi yake kuhusu vyeti hivi vya kughushi vimekiri kuwa vyeti
hivyo ni vyao.
Hili
ni tatizo kwa kweli,” alisema Daudi. Katibu huyo alisema baada ya ajira
kufunguliwa katika mwaka wa 2017/18, sekretarieti hiyo imepokea vibali
vya ajira 292 vyenye jumla ya idadi ya nafasi 2,611 na hadi kufikia
Septemba mwaka huu, waombaji 185 wameshapangiwa vituo vya kazi.
“Katika
juma lijalo tunatarajia kuwapangia vituo vya kazi zaidi ya wasailiwa
400 ambapo pia tuna vibali vingi ambavyo vipo kwenye hatua mbalimbali,”
alieleza. “Naomba niweke wazi kuwa chombo hiki hakikuanzishwa kwa bahati
mbaya, kilianzishwa kwa ajili ya kutatua changamoto za ajira nchini
kutokana na matatizo kadhaa yaliyokuwepo huko nyuma kama vile kuajiri
bila kuzingatia sifa, ukabila, udini, undugu na urafiki, na gharama
kubwa za matangazo ya ajira,” alieleza.
Pamoja
na hayo, waziri huyo aliagiza sekretarieti hiyo, kuhakikisha inafanya
mchakato wa ajira kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za ajira
zilizopo na kupata watumishi wa umma wenye sifa stahiki, hivyo kuisaidia
Serikali kutekeleza mipango yake ya kiuchumi na kimaendeleo.
“…Naomba
muendelee kuwa wabunifu na kutumia mbinu za kisasa katika kutekeleza
majukumu yenu ili rasilimali watu mnayoiandaa ikidhi matarajio ya wadau
wenu pamoja na taifa kwa jumla,” alisema Waziri Kairuki. Alisema chombo
hicho kikitoa wasailiwa bora wanaokidhi mahitaji ya waajiri, watasaidia
taifa kufikia malengo iliyojiwekea ikiwemo kuijenga Tanzania.
0 comments: