1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likae
kama Kamati ya Mipango ili kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango
na Bajeti kwa Mwaka 2018/19.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutujalia uzima na afya. Aidha, tunamshukuru sana kwa
kuendelea kulijalia Taifa letu amani na utulivu na kutuwezesha kukutana
katika mkutano huu wa tisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ili kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
3.
Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea
kuniamini kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango kufuatia mabadiliko
aliyoyafanya hivi karibuni katika Baraza lake la Mawaziri na safu ya
uongozi wa Mikoa. Aidha, ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Naibu
Mawaziri na Wakuu wa Mikoa waliobakia katika nafsi zao na wale
waliobadilishwa vituo vya kazi. Vile vile, ninawapongeza kwa dhati wote
walioteuliwa kuwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wakuu wa Mikoa wapya.
4.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nitumie fursa hii adhimu kutambua na
kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na makini katika
kusimamia rasilimali za Taifa, kupambana na rushwa, kuimarisha nidhamu
na uwajibikaji katika utumishi wa umma na zaidi ya yote, kwa moyo wake
adili katika kupatia majibu kero za wanyonge. Hakika uongozi wake
umezidi kuijengea heshima kubwa nchi yetu.
5.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mhe. Janeth
Masaburi (Mb) aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge
lako Tukufu hivi karibuni kutoka Chama Tawala cha CCM. Aidha,
nawapongeza kwa pamoja Waheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Kiza
Hussein Mayeye, Nuru Awadh Bafadhili, Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz
Mtamba, Sonia Jumaa Magogo, Rehema Juma Migilla na Zainab Mndolwa Amir
walioteuliwa na Chama cha Wananchi - CUF kuwa Wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninapenda kuwakaribisha na kuwashauri
watumie jukwaa hili kikamilifu katika kuishauri Serikali na kuwatumikia
wananchi. Napenda pia kumpongeza Bw. Stephen Kagaigai kwa kuteuliwa na
Mheshimiwa Rais kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
6.
Mheshimiwa Spika, ninawiwa pia kutoa shukrani za dhati kwa Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb) na
watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu,
Bw. Doto Mgosha James kwa ushirikiano walionipa katika maandalizi ya
hotuba hii na vitabu vya Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo. Aidha,
ninawashukuru sana Wizara, Taasisi, Idara za Serikali, Sekta Binafsi na
wadau mbalimbali waliotoa maoni na michango yao katika kukamilisha
Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo.
0 comments: