Vigogo wanne Tanesco Wapandisha Kizimbani Wakikabiliwa na Makosa 202 Ya Uhujumu uchumi


Maofisa wanne wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco )na watu wengine wawili, leo Novemba 7, 2017 wamepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka 202 ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya bilioni 2.7.

Hati ya Mashtaka imesomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi aliyekuwa akisaidiana na wakili wa serikali Gloria Mwende ambapo watuhumiwa wote wanakabiliwa na shtaka moja la kula njama, kutoa taarifa za uongo, kuisababishia hasara serikali na mashtaka 199 ya wizi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa washtakiwa hao ametajwa kuwa ni, Afisa Mapato Mwandamizi, Emmilian Mlowe, Mhasibu wa Mapato msaidizi, Shakira Ngella,  meneja wa fedha mwandamizi Mkama Maira na Mhasibu wa udhibiti wa Mikopo Yaned Jonas.

washtakiwa wengine ni, Bashiru Ngella na Barnabas Massaly.

Imedaiwa kuwa, kati ya Januari 7, 2014 na Januari 31,2015 jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote hao walikula njama ya kutenda kosa la wizi.

Katika shtaka la pili, imedaiwa kuwa, tarehe hizo, katika ofisi ya Tanesco Kinondoni, iliyopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa, Mlowe,Ngella,  Maira na Jonas wakiwa ni waajiriwa wa Tanesco Kinondoni, wakiwa na uwezo wa kuingia katika mfumo wa kompyuta unaojulikana kama Tansms33, wakiwa na nia ya kulaghai walifanya maingizo ya uongo katika mfumo huo ya kiasi cha  Sh 2,746,485,545.63 wakijaribu kuonyesha kuwa fedha hizo zililipwa kwa Tanesco  na mawakala wa tatu (Luku Vendos) kama manunuzi ya umeme wa Luku (unit).

Katika shtaka la 202 washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kusababisha hasara ambapo wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi ,2014 na Machi 31,2016 washtakiwa hao kwa matendo yao waliisababishia Tanesco kupata hasara ya Sh 2,746,485,545.63/-. 
Washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea kitu chochotemahakamani hapo kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa upande wa Mashtaka, upelelezi wa kesi huyo bado haujakamilika na washtakiwa wamerudishwa rumande hadi Novemba 2, mwaka huu. 
Hakimu Nongwa amewashauri washtakiwa hao kuomba dhamana katika Mahakama Kuu kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi.
Share on Google Plus

0 comments: