Waziri Wa Afya Azungumzia Upungufu wa Dawa Nchini


Waziri wa Afya, Jinsia, watoto na wanawake Mheshimiwa Ummy Mwalimu, amesema kwa sasa nchi haina tatizo la upungufu wa madawa, kama ambavyo wengi wanadai.

Akijibu swali la Waziri Kivuli wa Afya, Mhe Dr Godwin Mollel Bungeni mjini Dodoma, na kusema kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. John Pombe Magufui, imehakikisha imeongeza bajeti ya dawa ili kuinua sekta ya afya nchini.

“Kwanza nataka kumsahihisha waziri kivuli jambo moja, hakuna upungufu mkubwa wa dawa Tanzania, na kati ya jambo kubwa ambalo Rais amelifanya ni kuongeza bajeti ya dawa, tusikariri taarifa zilizopitwa na wakati, kama mnataka kumtendea haki Rais Magufuli, mtendeeni kwa kumpima ni kiasi gani amewekeza katika upatikanaji wa dawa”, amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy ameendelea kwa kusema kwamba sasa hivi serikali imejidhatiti katika kuhakikisha inakabiliana na kutoingiza dawa ambazo zinakaribia kuharibika, na kuingia hasara kuziteteketeza huku ikisema changamoto kubwa huwa inajitokeza kwa dawa za misaada, kitu ambacho wameshaacha kufanya hivyo.

“Tanzania dawa zinazochina ni1.8% tuko chini ya kiwango cha kimataifa cha 5%, kuna tatizo kubwa la maoteo, watu hawaleti mahitaji halisi ya dawa, dawa nyingi zinazochina ni za misaada, unakuta tumenunua dawa za kutibu malaria, unaletewa tena dawa za misaada, tumechukua miongozo sasa hivi hatuchukui dawa za misaada ambazo zimekaribia kuharibika au tayari tunayo kwenye bohari yetu ya dawa”, amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Majibu hayo yalikuja mara baada ya Mbunge Godwin Mollel kuuliza swali la nyongeza linalosema “katika nchi ambayo kuna upunufu wa dawa na kuna dawa zinaharibika huku tukitumia mabilioni kuteketeza, haoni kama kuna ufisadi unaofanyika?”.
Share on Google Plus

0 comments: