Buriani BABU: Nimjuavyo Samwel John Sitta.
Alfajiri ya leo, Novemba 7, 2016 imekuwa siku ya huzuni na
majonzi makubwa kwa Taifa. Tuliamka na kukutana na habari za kusikitisha
juu ya kifo cha Mzee wetu Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mzee Sitta alikuwa mgonjwa kwa kitambo
kidogo, lakini bado tulikuwa na matumaini kuwa afya yake ingetengamaa na
kuendelea kuwa nasi.
Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT WAZALENDO.
Habari hizi za kufariki dunia kwake zilizosambaa kwa kasi
kubwa kupitia mitandao ya kijamii zimetushtusha mno. Hatimaye taarifa
rasmi ikatoka kuthibitisha habari hizo. Kuwa Mzee watu amefariki dunia
akiwa kwenye matibabu nchini Ujerumani.
Samwel John Sitta aliitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na
kwa uadilifu mkubwa sana. Si hivyo tu, sisi wengine pia kwa kiasi flani
Hata kukua kwetu kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi
yetu alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika tanzia hii ninamkumbuka Mzee Sitta Kwa namna nilivyofungamana
naye binafsi na namna nilivyomshuhudia katika kazi zake mbalimbali za
uongozi.
Samwel Sitta ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa
Babu yangu. Tukiwa Bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo
'babu' kwa mwandiko wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa.
Labda siku za usoni 'vinote' (vimemo) hivi vinaweza kuchapishwa pindi
watafiti watakapokuwa wakiandika historia ya nchi yetu na Bunge letu.
Hivyo siku zote za maisha yetu nilimuita babu.
Disemba 29, 2005 mzee Sitta aliniapisha kiapo cha ubunge
tarehe. Maneno ambayo aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge na
Katiba ya Nchi niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku
hiyo hiyo jioni. Baada ya kula kiapo cha Utii na cha uaminifu kawaida
Wabunge hupewa mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi.
Kwangu haikuwa hivyo, Mzee Sitta alinikumbatia na kuniambia
"Utakuwa Kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future
(unayo kesho njema)". Maneno haya hayajawahi kunitoka katika kumbukumbu
zangu, ni maneno ya faraja na msukumo wa kunitaka kwenda mbele kila
ninapopata misukosuko ya kisiasa. Mara kadhaa yeye mwenyewe alikuwa
akinipigia na kunikumbusha juu ya maneno yake haya na kunitia moyo.
Babu Sitta alikuwa Mlezi wa wanasiasa vijana, binafsi
amenilea na kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Kidato cha
Tano (Form Five) katika Shule ya Sekondari ya Galanos ya jijini Tanga,
nikisomea mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE). Hali ya hewa
ya jiji la Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwa mara kwa mara. Lakini
pia sikupenda kusoma HGE, nilitaka kusoma Hisabati badala ya Historia.
Wakati wa likizo ya mwezi Disemba mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda
Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo
la Hisabati kidato cha Tano na Sita. Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa
kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati ule, ndugu Ndeki alisoma
pamoja na Samwel Sitta.
Marehemu Samuel SittaSamuel Sitta .
Kipindi hicho Mzee Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments
Promotion Centre (IPC) mara kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania
Investments Centre (TIC) mara baada ya kuwa mbunge wa Urambo kwa miaka
20 (1975 - 1995). Nikaenda Ofisi za IPC, zilizokuwa mahala ambapo leo ni
Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe. Nilipofika Katibu Muhtasi wake
akaniuliza kama nina miadi na bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia
hawezi kukuona. Nikasisitiza sana na kumlilia dada yule aniruhusu hata
kwa akika chache tu. Akaniruhusu.
Nilipofika Mzee Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima
kubwa. Nikamwambia kwamba ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu
ya Kidato cha Nne, nikampa maana nilikuwa natembea nayo. Alipoyasoma
akaniambia, "wewe hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo
yako unaweza kusoma shule yeyote nchini ya chaguo lako". Akainua simu
akampigia ndugu Ndeki kumuomba anihamishe.
Kisha akaniandikia kikaratasi niende Wizarani muda ule ule.
Nilipofika Wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari
Mazengo. Nilipotoka nje ya Wizara nikakutana na kijana mwengine, Godfrey
Hiluka, anaomba uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda
Tosamaganga Iringa. Akaniambia, achana na Mazengo hakuna Mwalimu wa
Uchumi na hali ya vyoo ni mbaya sana.
Nikarudi kwa Mkurugenzi. Mtumishi aliyenijazia fomu za
Uhamisho (Mzee wa Makamo) aliponiona narudi na kumwambia sitaki kwenda
Mazengo, akachukua fomu zangu za uhamisho na akachukua 'kifuta - wino'
(whiteout) akafuta Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira
"nyie watoto wa wakubwa bwana!"Sikujali nikaenda zangu Tosamaganga
kusoma Uchumi, Jiografia na Hisabati (EGM).
Samwel John Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo yangu
shuleni, mpaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Taasisi ya InWent
nchini Ujerumani. Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara
ya Kimataifa mwaka 2004 nilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma.
Nikachagua kuunganisha makampuni ya Kijerumani na makampuni ya Tanzania
kwa kuandika mradi wa kuchukua wafanyabishiara 20 kutoka Tanzania na
kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Ilibidi kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na
Mzee Sitta akawa mstari mbele kuhakikisha Mradi unafanikiwa na
tukautekeleza kwa umakini kwa msaada wa afisa wa TIC aitwaye Phina
Lyimo. Mafungamano yetu hayakuishia hapo, mwaka mmoja baadaye tukakutana
na Mzee Sitta Bungeni, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki
na mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake kwangu
ukaendelea mpaka mauti yalipomkuta leo mapema asubuhi. Taifa limepoteza
Kiongozi mzalendo, lakini mimi nimepoteza pia 'babu Mlezi'.
Samwel John Sitta alikuwa Mwanamageuzi (Reformer), na
kupitia uanamageuzi wake alifanya mabadiliko makubwa sana katika
uendeshaji wa shughuli za Bunge akiwa Spika wa Bunge kwa miaka mitano.
Sisi tuliohudumu kwenye Bunge la tisa chini yake, tukimwita Spika wa
Viwango na Kasi, tuliona wenyewe juhudi zake za kuliweka Bunge katika
nafasi yake ya Kikatiba.
Licha ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Wabunge yanakuwa
yanayolingana na hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge
linaisimamia Serikali sawa sawa. Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa
na mvutano mkubwa sana kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu Edward Lowasa
katika kuleta mabadiliko hayo.
Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano ule ulitokana na tetesi
kwamba Sitta ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo
badala yake. Sio Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha
tetesi zile. Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Edward Lowasa
ataweza kusemea hili siku za usoni.
Samwel Sitta alitumia fursa ya msuguano huo kufanya
mabadiliko makubwa ya kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo
ndani ya Bunge na kuhakikisha kuwa Taarifa za Kamati za Bunge, hususan
Kamati za Usimamizi wa Serikali, zinakuwa zinasomwa na kujadiliwa ndani
ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni.
Wakati wa Bunge la 8 chini ya mzee Pius Msekwa, Taarifa za
CAG hazikuwahi kusomwa hata mara moja bungeni. Ni kutokana na mabadiliko
haya ya kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC ) ilianzishwa mwezi Machi, mwaka 2008. Nilichaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ile na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi
ya Bunge ambayo kipindi hicho tuliiona kama Kamati ya Wabunge wazee.
Namna nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa POAC nayo ni hadithi
nyengine ya namna ya malezi ya kiuongozi yalifanywa na Spika Sitta.
Sikuwa nimejaza fomu kuomba hata ujumbe wa Kamati ya POAC. Wakati huo
ulikuwa ni wakati wa vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa
na Waziri wa Nishati Hotelini nchini Uingereza kwa siri).
Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani
(Kamati iliyoundwa na Rais kuchunguza mikataba na sheria za madini)
nikiwa na Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige. Spika wa Bunge akanipigia
simu, akaniambia "Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge.
Nimekuteua Kamati ya POAC ambayo ni Kamati mpya itakayokuwa chini ya
Kambi ya Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa Kamati hii, lakini
nahitaji damu changa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge. Naomba
unikubalie na kesho uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na
ugombee. Utashinda maana nimeshafanya kazi yangu".
Sikuwa na namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea
kuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya marehemu Abdallah
Kigoda, ama Kamati ya Nishati na Madini chini ya Mzee William
Shelukindo.
Lakini ombi la Mzee ni amri. Nikawa Mwenyekiti wa POAC na
kuwa mmoja wa washauri wakuu wa Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa
chini ya Mzee John Momose Cheyo na Kamati ya LAAC ikawa chini ya Dkt.
Willibrod Peter Slaa. Ilikuwa ni Bunge lenye meno kweli kweli.
Spika Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimpelekea kufanya
maamuzi ambayo wakati mwengine yalimweka kwenye matatizo na wananchi.
Mfano mzuri ni masuala ya 'Hoja Binafsi ya Buzwagi' na 'Hoja ya Wizi wa
Fedha Benki Kuu (EPA)'. Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa Wabunge wenye
hoja hizo, yaani mimi na Dkt. Wilbroad Slaa kiasi cha kuziboresha hoja
zile kwa kalamu yake mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa wanapenda
hoja hizi na hivyo Waziri Mkuu Edward Lowasa akamweka kwenye wakati
mgumu sana wa kuegemea upande wa Serikali.
Hoja ya dkt Slaa akaitupa kuwa 'Ni makaratasi ya
kuokoteza'. Hoja yangu akaiingiza Bungeni na akasimamia kusimamishwa
kwangu Bungeni baada ya kuwasilisha hoja hiyo. Wananchi walimkasirikia
sana. Siku moja usiku, nikiwa nyumbani kwa ndugu Freeman Mbowe
Mikocheni, Spika Sitta akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu
wanamtukana kwa ujumbe wa simu (sms), akanitaka niwakataze. Nilimkubalia
tu, lakini sikuwa na uwezo huo. Nchi ilikuwa imevimba. Ilikuwa Oktoba
2007. Samwel Sitta alijua namna ya kuisoma nchi, na akamua kuwapa
wananchi watakacho, wakati mwengine.
Mwezi Novemba, katika kujibu kiu ya wananchi kuhusu
uwajibikaji na kufuta makosa ya Buzwagi na EPA, Spika alisimamia kuundwa
kwa Kamati Teule kuchunguza suala la Mkataba wa Richmond. Yaliyofuata
yalikuwa historia. Taarifa ya Kamati Teule husika ilipelekea kuanguka
kwa Serikali kwa mara ya kwanza katika hsitoria ya Tanzania. Waziri Mkuu
Edward Lowasa alilazimika kujiuzulu ndani ya Bunge, Baraza la Mawaziri
likavunjika na Serikali mpya kuundwa chini ya Waziri Mkuu mpya, ndugu
Mizengo Pinda. Spika Samwel Sitta akawa ni Spika wa pili wa nchi yetu
aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano ya uspika
wake.
Mzee Msekwa yeye alikaa kwenye Uspika kwa miaka 13. Miaka
10 na Waziri Mkuu mmoja, ndugu Sumaye. Akianzia Uspika Mwaka 1993. Mwaka
mmoja mbele akishuhudia mabadiliko ya Mawaziri Wakuu, kutoka mzee John
Malecela kwenda kwa mzee Cleopa Msuya. Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa,
Samwel Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa Viwango mpaka
alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.
Sifa nyengine ya Spika Sitta ni Uungwana, alikuwa mwepesi
mno wa kuomba msamaha pale alipokosea. Nakumbuka siku moja mwaka 2009
alimfukuza Bungeni Mzee mwenzake John Cheyo kwa makosa ambayo Mzee Cheyo
hakufanya. Baadhi yetu tukakasirishwa sana na kitendo kile. Nikaenda
kumwona Mzee Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake
namna ile. Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi John Cheyo.
Tukiwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge, kwa ajenda zake za kawaida tu,
Mzee Sitta akamwomba radhi Mzee Cheyo.
Nikikumbuka kisa hiki hutabasamu, maana Jaji Werema,
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicheka mpaka kuanguka chini.
Sababu? Mzee Sitta aliketi kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa Kamati
tukiwa tumetulia tuanze kikao. Mzee Sitta akasema "John, naomba radhi
kwa tukio lililotokea Bungeni wiki iliyopita. Sijui nilikuwa nina nini
siku hiyo?, nadhani nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka
kunitoa, nisamehe Mzee mwenzangu".
Zitto Kabwe. akiwaza
Kicheko ukumbi mzima na mzee John Cheyo akamkubalia radhi
yake huku naye akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika
pamoja Kitabu "Bunge lenye Meno".
Nimwelezeje zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika wa Kasi na
Viwango Samwel John Sitta? Mwanasiasa Shupavu, Jasiri, Mwenye Ngozi
Ngumu, Mbabe, Mnyenyekevu inapobidi na mwenye Uthubutu. Tangulia Babu.
Tangulia Mjukuu wa Fundikira. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John
Sitta. Ingawa umeondoka duniani, bado unaishi kupitia kazi zako za
Kizalendo kwa Nchi yetu.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Novemba 7, 2016
Dodoma
0 comments: