Mbunge
wa Chadema wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari ameweka rehani ubunge
wake baada ya Rais John Magufuli kumpokea aliyekuwa diwani wa chama
hicho aliyejiuzulu akisema ni kwa sababu ya kuunga mkono juhudi za Rais.
Nassari amedai ana ushahidi wa kielektroniki unaoonyesha madiwani hao walivyopewa rushwa ili wajiuzulu nafasi zao.
Hata
hivyo, diwani wa Kata ya Kimandolu, Mchungaji Rayson Ngowi ambaye
amepokewa na Rais Magufuli juzi baada ya kujiuzulu Chadema akizungumzia
tuhuma hizo alisema madai hayo hayana ukweli wowote na kama Nassari ana
ushahidi ni vyema angeutoa hadharani.
Ngowi
aliwashauri Chadema mkoani Arusha watatue matatizo yaliyopo ndani ya
chama hicho na wasitafute visingizio kwa kuwa yeye ameamua kujiuzulu kwa
kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na hajapewa rushwa yoyote.
Diwani
mwingine aliyejiengua katika chama hicho wa Kata ya Muriet, Credo
Kifukwe alisema hakuna chochote alichopewa kama rushwa kwa lengo la
kujiuzulu, akimshauri Nassari autoe hadharani ushahidi anaousema na si
kushusha tuhuma zisizo na mashiko.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini hapa, Nassari alisema ushahidi huo
ameuhifadhi ndani ya ‘flash disc’ na yuko tayari kumkabidhi Rais
Magufuli na vyombo vya uchunguzi.
Mbunge huyo alisema endapo ikithibitika kuwa ushahidi wake ni wa uongo yuko tayari kujiuzulu nafasi yake ya ubunge.
“Ninao
ushahidi na kama Mheshimiwa Rais yuko tayari niko tayari kumpatia
ninayo flash, ushahidi ninao kwa muda mrefu na tulijua watapokelewa juzi
madiwani wawili lakini mmoja amekataa akaenda mmoja,” alisema Nassari.
Alidai
kwamba kwa kipindi kirefu alipokuwa masomoni nchini Uingereza alikuwa
akijiuliza ni kwa nini madiwani katika Mkoa wa Arusha wamekuwa
wakijiuzulu na ndipo alipoamua kufanya uchunguzi wa kina.
Nassari
akiwa ameambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema katika
mkutano huo, alisema alianza kufanya uchunguzi Mei kwa kutumia vifaa vya
kielektroniki alivyovinunua nchini Uingereza na kubaini kwamba baadhi
ya madiwani wanaojiuzulu walipewa rushwa ya fedha, ahadi ya vyeo na ya
makazi.
Alisema
uchunguzi juu ya tuhuma za madiwani hao kujiuzulu aliufanyia ndani ya
ofisi ya umma akisisitiza hakuna diwani wa Chadema mkoani Arusha ambaye
amejiuzulu kwa kumuunga mkono Rais Magufuli bali wamepewa rushwa.
“Mheshimiwa
Rais anapambana na rushwa lakini kuondoka kwa madiwani ni mfumo wa
rushwa anaopambana nao niko tayari kujiuzulu nafasi yangu ya ubunge
endapo ikithibitika ushahidi wangu ni wa uongo,” alisema Nassari.
Madiwani
wapatao 10 wa Chadema wamejiuzulu kwa nyakati tofauti. Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ameshawahi kunukuliwa
akikanusha tuhuma za kupewa rushwa madiwani wanaojiengua kutoka Chadema
na kujiunga na CCM.
Polepole
Julai alikaririwa akisema iwapo Chadema ina viongozi wanaoweza kuhongwa
na wakahongeka basi ni chama cha ovyo kwa kuwa chama kilicho imara na
watu wake wapo safi hawawezi kuhongeka.
0 comments: