MAHAFALI YA PILI YA KIDATO CHA SITA WAMA NAKAYAMA YAFANA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewahimiza wanafunzi kote nchini kupenda kusoma masomo ya Sayansi hasa watoto wa kike ili Taifa liweze kujitosheleza kwa wataalamu wa fani mbalimbali nchini hasa wakati huu ambao Taifa linaelekea kwenye uchumi wa Viwanda.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwenye mahafali ya Pili ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wa shule ya sekondari ya WAMA- NAKANYAMA Jijini Dar es Salaam, mahafali ambayo imehudhuriwa na wake wa Marais Wastaafu.

Makamu wa Rais amesema haitapendeza hata kidogo ajira nyingi nchini kuchukuliwa na wataalamu mbalimbali mataifa ya nje hasa kipindi hiki wakati Serikali inahimiza ujenzi wa viwanda hivyo amesisitiza wanafunzi wajikite kwenye kusoma masomo ya sayansi ili taifa liweze kujitosheleza kwa ajili ya manufaa ya maendeleo ya taifa. Amesema katika kuhakikisha taifa lipata wanasayansi wengi, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa maabara na kununua vifaa vya maabara ili kuhamasisha wanafunzi wengi zaidi kupenda kusoma masomo ya sayansi kote nchini.

Makamu wa Rais pia amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Tano inakusudia kuimarisha ufundishaji wa masomo ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano –TEHAMA- katika shule za Sekondari na kujenga maabara za kompyuta nia ikiwa ni kuongeza wataalamu wa fani hiyo nchini. Kuhusu mila na desturi kandamizi kwa wanawake na wasichana zilizopo kwenye baadhi ya jamii nchini, Makamu wa Rais ameitaka jamii kukomesha mila hizo na iwashirikishe wanawake katika mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi kwani watakuwa ni chachu ya maendeleo katika jamii husika.

“Wote tunajua wanawake ni chachu na kiungo muhimu katika maendeleo ya jamii, Taifa na Dunia kwa ujumla hivyo ni wajibu wa jamii kushirikisha wanawake katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo kote nchini” amesisitiza Makamu wa Rais.



Makamu wa Rais pia ameipongeza Taasisi ya Wanawake na Maendeleo – WAMA- kwa kujenga shule Mbili za Sekondari na kusomesha watoto wanaotoka kwenye familia maskini na yatima na kusema huo ni mfano wa kuingwa na wadau wengine wa maendeleo katika kusaidia kundi hilo ili watoto wanaotoka kwenye familia maskini nao waweze kuapata elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya baadae. 


Kuhusu changamoto zinazoikabili shule ya WAMA – NAKAYAMA, Makamu wa Rais ameahidi kushughulikia changamoto hizo ikiwemo uhaba wa maji, ubovu wa barabara kuelekea kwenye shule hiyo na tatizo la uhaba wa mabweni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WAMA na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mama SALMA KIKWETE amesema aliamua kuanzisha taasisi hiyo ambayo inamiliki shule Mbili mpaka sasa ili kusaidia watoto wa maskini na yatima kupata elimu bure ambapo mpaka sasa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaliohitimu katika shule hizo ambao wamejiunga na masomo ya elimu ya juu.

Mama Salma Kikwete ameshukuru ushirikiano mkubwa anaopata kutoka Serikalini unaolenga kuhakikisha shule zinazoendeshwa na taaisisi hiyo ikiwemo ya Wama – Nakayama zinafanya vizuri.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete pamoja na viongozi wengine wakiangalia kwa vitendo majaribio ya kiyasansi kutoka kwa wanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya WAMA NAKAYAMA kwenye sherehe za mahafali yao ambapo wanafunzi 45 wamehitimu. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete(kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa WAMA Bi.Zakhia Meghji wakiimba wimbo maalumu wa shule ya Sekondari ya WAMA NAKAYAMA wakati wa mahafali ya pili ya kidato cha sita ambapo wanafunzi 45 wamehitimu.
Baadhi ya Wanafunzi waliohitimu kidato cha sita katika shule ya sekondari WAMA NAKAYAMA.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wateule

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba amekutana na kufanya mazunguzo na Mabalozi Wateule wanaoenda kuiwakilisha Tanzania maeneo mbalimbali Duniani.Mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwake Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma, yalijikita katika kujadili namna bora ya kuiwakilisha Tanzania ughaibuni kwa kuzingatia sera ya nchi ya mambo ya nje, kwa lengo la kuboresha mahusiano ya Kidiplomasia baina ya Tanzania na nchi hizo, na kwa kuzingatia maslahi mapana ya kiuchumi ya nchi yetu ikiwemo kutangaza shughuli za utalii zinazopatikana nchini.


Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisisitiza jambo 


Balozi Mteule Baraka H. Luvanda akichangia jambo wakati wa mazungumzo. Punde baada ya mazungumzo na Mhe. Naibu Waziri, Mabalozi walikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Katibu Mkuu Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt.Aziz P Mlima akiongea na Mabalozi ofisini kwake mjini Dodoma

Mazunguzo yakiendelea

Prof. Kitila asaini kandarasi za zaidi ya bilioni 600 kupeleka maji Tabora na Shinyanga vijijini

https://swahilitimes.com/wp-content/uploads/2017/04/mkumbo.jpgKatibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo amesaini kandarasi zenye thamani ya dola za Marekani Milioni 268.35 ambazo ni zaidi ya Shilingi bilioni 600 za Tanzania mjini Tabora kwa mkopo wa benki ya Exim ya nchini India kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzani kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kutoa Ziwa Victoria na kupeleka katika Manispaa ya Tabora na Halmashauri za Igunga, Uyui, Shinyanga Vijijini na Nzega. 

Utekelezaji wa mradi ni wa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ya Mradi ilikuwa kufanya usanifu na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi, kazi ambayo ilifanywa na Kampuni ya WAPCOS Ltd ya India na ilikamilika mwezi Desemba 2015. 

Awamu ya pili ni ujenzi wa mradi ambao umegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza itaanzia Kijiji cha Solwa (kilichopo Wilaya ya Shinyanga Vijijini) hadi Mji wa Nzega, ujenzi utafanywa na Kampuni ya Megha Engineering Infrastructures Ltd ya India. Sehemu ya Pili inaanzia Mjini Nzega mjini hadi Manispaa ya Tabora kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, ujenzi utafanywa na Kampuni ya L&T ikishirikiana na kampuni ya Shriram zote kutoka India.
Sehemu ya tatu inaanzia Nzega mjini hadi Igunga mjini, ujenzi utafanywa na Kampuni ya Afcons ikishirikiana na kampuni ya SMC zote kutoka India. Usimamizi wa mradi unafanywa na Kampuni ya WAPCOS Ltd ya India.

Katibu Mkuu Wizara ya maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo naVisay Uplenchwar wa Kampuni ya Megha Engineering Infrastructures Ltd akisaini Mikataba ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka kijiji cha Solwa Shinyanga na kupeleka maji Nzega.Mbunge wa Nzega Hussein Bashe akimsalimia waziri wa Maji na Umwagiliaji Eng. Lwenge
 Waziri
wa maji na Umwagiliaji Eng. Gerson Lwenge akipokewa na Mkuu wa Mkoa wa
Tabora wakati alipowasiri katika viwanja vya Furahisha Tabora.

RC MAKALLA APOKEA MSAADA WA MIFUKO 400 YA SARUJI KUTOKA AKIBA COMMERCIAL BANK

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Mh.Amos Makalla amepokea msaada wa mifuko 400 ya saruji,kutoka kwa Benki ya AKIBA Commercial Bank Ltd ,kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa njia za Wagonjwa,yenye urefu wa mita 175 katika hospitali ya Mkoa wa Mbeya.

Akizungumza hayo jana jijini Mbeya wakati wa kupokea msaada huo,RC Makalla aliwashukuru Wadau hao kwa kujitolea na kulishughulikia ombi lake kwa haraka na kwa uzito wa juu kabisa.

"Nawashukuru sana Wadau AKIBA Commercial Bank Ltd , kwa kulishughulikia ombi langu hili, ambalo sikutarajia kama lingechukua muda mfupi hivi,nawashukuru sana na nawaomba msichoke na  tuendelee kuijenga Mbeya yetu kwa pamoja",alisema Makalla.

Makala alisema kuwa kupitia kwa marafiki wa hospitali ya Mkoa,wanaoishi ndani na nje ya mkoa huo,kupitia harambee walioifanya hivi karibuni wamefanikiwa kukamilisha ujenzi wa mita 55 na na kuwa awamu ya pili inaendelea kwa ujenzi wa mita 175.

Mh.Makalla alisema kuwa katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo,zilitumika fedha jumla ya shilingi milioni 600,kutokana na mahitaji kuwa makubwa ya ujenzi,ujenzi  ukasimama. kwa sababu zilikuwa zikihitajika fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni 55,ndipo wakachukua hatua za kuomba msaada zaidi kwa wadau ambao ni AKIBA Commercial Bank Ltd .

"Kukamilika kwa ujenzi huu kutaondoa tatizo la wagonjwa kupelekwa au kwenda wodini kwa taabu, kwani wakati wa mvua tatizo linakuwa kubwa ",alisema Mh Makalla.

Kwa upande wa Akiba Commercial Bank kupitia kwa Afisa Masoko na Uendeshaji Bi Dora Saria amesema waliguswa sana baada ya kuombwa na Mkuu wa Mkoa kutokana na wananchi kupata shida hasa wagonjwa kwenda wodini au kupeleka maiti kwenye chumba cha kuhifadhia maiti

Hivyo wao kama taasisi ya Benki waliguswa na jambo hilo,na wakachukua hatua ya kuchangia shilingi milioni 5 sawa na Mifuko 400 ya saruji na kuahidi kutoa Mafunzo na mikopo kwa wajasiriamali
Aidha Akiba wamevutiwa na jitihada za Mkuu wa Mkoa kuliweka jiji safi hivyo watatoa Vifaa vya usafi na kushiriki kufanya usafi mwisho wa mwezi huu.


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Mh.Amos Makalla akikabidhiwa mifuko 400 ya saruji na Bi. Dora Saria ambaye ni Afisa Masoko wa Akiba Commercial Bank Jijini Mbeya.Na Mr.Pengo wa Globu ya jamii Mbeya

RC Makalla akitoa neno la shukrani mbele ya Viongozi na wafanyakazi wa Benki ya Akiba na Serikali kwa ujumla.

KAMA ILIKUPITA BASI USILALAMIKE.......

HII HAPA ORODHA YOTE YA MAJINA 65 YA PAUL MAKONDA KUHUSU MADAWA YA KULEVYA

 
Orodha ya majina yote 65 yaliyotamkwa leo tarehe 08.02.2017 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda wanaojihusisha na Dawa za kulevya hii hapa.

BAADA YA SOMALIA KUPATA RAIS MPYA: Mambo usiojua kuhusu rais mpya wa Somalia


Rais mpya wa Somalia Mohamed Abdullahi MohammedRais mpya wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohammed
 Rais mpya wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohammed anaitwa 'Farmajo' baada ya chakula cha Kitaliano cha Jibini
Inasemekana kwamba alipenda sana kula Jibini wakati alipokuwa kijana wakati wa ukoloni wa Italiano
Ana uraia wa nchi mbili za Marekani na Somalia na anajulikana kwa kampeni yake ya kupigania haki za kibinaadamu.
Amewahi kuhudumu kwa muda mfupi kama waziri mkuu mwaka 2011 lakini akajiuzulu baada ya miezi michache kufuatia migogoro kati yake na aliyekuwa rais Sheikh Sharrif hassa.

Hakuwa maarufu na wanasiasa wengine kwa kuwa alijionyesha kuwa mtu wa watu akipanda ndege za bei ya chini wakati alipokuwa akisafiri katika mataifa ya ughaibuni.
Miongoni mwa wagombea wote 20 ndiye aliyekuwa maarufu katika mtandao wa kijamii.
Wapinzani wake walikosolewa kwa kuungwa mkono na Kenya na hata Ethiopia.
Wafuasi wake wanapinga mataifa ya kigeni kuingilia kati utawala wa Somalia na wanataka kuona mabadiliko nchini humo

KUELEKEA UBUNGE WA AFRIKA MASHARIKI

UBUNGE BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI: WATANZANIA WATAKIWA KUTOA MAONI

Wananchi mbali mbali wanashauriwa kuanza kutoa maoni yao juu ya nani na nani wanastahili kuwa wabunge wa Bunge la Africa Mashariki bunge ambalo uchaguzi wake unatarajiwa kufanyika mwezi april mwaka huu katika kikao cha bunge la bajeti kutokana na kanuni za bunge hilo linalowataka wabunge wake kupatikana kwa kupigiwa kura na wabunge wa nchi wanachama.

kwa mtazamo wako nani anastahili kuwa mbunge na nani hastahili?, ili kutoa maoni yako hayo juu ya  mtu unayetaka au unayehisi anastahili kuwa mbunge wa Bunge lijalo la Afrika mashariki tafadhali Tuma email yako katika anuani yetu ya EMAIL: jamvilahabari@gmail.com
nasisi tutakusanya matokeo yote na kuyatoa kwa umma